Wagombea Urais UKAWA bado? Wajawazito feki kwenye BVR, Rufaa ya akina Mramba..
MWANANCHI
Wakati leo saa 10 jioni ndiyo muda wa
mwisho uliopangwa kurejesha fomu za kuomba kuteuliwa kuwania Urais ndani
ya CHADEMA, hadi sasa hakuna mwanachama hata mmoja aliyejitokeza
kuzichukua.
Hali hiyo inazidisha sintofahamu
iliyougubika mchakato wa Urais ndani ya chama hicho na ndani ya UKAWA,
kuwa huenda kuna ‘mtu wa nne’ anayesubiriwa kutoka nje ya chama hicho
japo kuhusu Viongozi na Wabunge wa chama hicho walisema Edward Lowassa anakaribishwa mradi tu afuate kanuni na taratibu.
Suala la mgombea Urais wa UKAWA
limeendelea kuteka mjadala wa kisiasa nchini huku Watanzania wakisubiri
kufahamu nani atateuliwa kupambana na Mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli.
Katika Mkutano wake uliofanyika Mwanza Jumatano Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe aliwaomba Watanzania wavumilie wakati wanakamilisha taratibu za kumpata mgombea Urais.
Pia, ilielezwa kuwa chama hicho kilikuwa
kinasubiri mkutano wa Baraza Kuu la Uongozi wa CUF unaofanyika leo,
huku taarifa nyingine zikisema chama hicho kilikuwa hakijampata mgombea
mwenza kutoka Zanzibar.
Ratiba ya kuchukua fomu za Urais na
kurudisha ilikuwa inaonyesha ni leo na hakukuwa na dalili zinazoonesha
watu kujitokeza kuwania nafasi hiyo ya juu.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu
alisema kuna marekebisho yamefanyika katika tarehe hiyo ya mwisho
kurejesha fomu ambayo yatatangazwa ndani ya siku mbili au tatu ambayo
yalilenga kupisha mchakato wa kura za maoni, baadae chama hicho kilitoa
taarifa ya kusogeza mbele tarehe ya kurudisha fomu hadi Julai 31, 2015
saa 10 jioni.
MWANANCHI
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la
Wapigakura kwa Mkoa wa Dar es Salaam, unaendelea pamoja na kujitokeza
kasoro kadhaa, ikiwa na pamoja na baadhi ya watu kutumia mbinu
mbalimbali ili kukwepa foleni.
Katika Kituo cha Bwawani Shule, Mtoni
Kijichi, wanawake wawili waliojifanya wajawazito walibainika kufanya
udanganyifu huo huku mmoja akiwa tayari amejiandikisha.
Hata hivyo, mmoja wa majirani ambaye anawafahamu, alidokeza kuwa anawafahamu wasichana hao na hawakuwa na wajawazito.
Mmoja alikuwa amekwishajiandikisha na aliwahi kuondoka mapema kabla ya mwenzake aliyekuja kwa staili hiyo na kushtukiwa.
Baada ya mzozo huo, aliondoka taratibu
eneo la tukio ndipo baadhi ya watu walipoanza kumkimbiza kubaini iwapo
ni mjauzito au la, msichana huyo alitoa makaratasi aliyokuwa ameyafunga
tumboni kama ujauzito na kuyatupa, huku akikimbia na kutokomea katika
vichochoro vya Mitaa ya Mtoni Kijichi.
Mmoja wa wasimamizi wa kituo hicho,
alisema kuwa hawana kawaida ya kuwakagua isipokuwa wanachoangalia ni
hali za watu wakiwamo wajawazito, walemavu, wazee na wenye watoto
wachanga.
Katika Vituo vingine baadhi ya wananchi
walilazimika kuzipiga kavukavu kutokana na wengine kutaka kuwapita
wenzao waliofika vituoni mapema.
NIPASHE
Mawaziri wa zamani, Basil Mramba na Daniel Yona jana
wamekata rufaa katika Mahakama Kuu ya Tanzania kupinga hukumu
iliyotolewa dhidi yao ya kwenda jela miaka mitatu na kulipa faini ya
Shilingi milioni tano.
Hukumu hiyo ilitolewa Julai 6 mwaka huu
na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kukutwa na hatia ya mashtaka
mawili ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara
ya Sh. bilioni 11.7.
Baada ya hukumu hiyo, jana Wakili wa Serikali, Timothy Vitalis
alisema Mahakamani hapo kuwa waliwasilisha maombi ya kukata rufaa
wakitaja upungufu wa aina tatu kwenye mwenendo wa kesi iliyopita kwamba
hati ya mashtaka haikuwa sahihi.
Alitaja eneo la pili lililosababisha
kukata rufaa kuwa ni ushahidi wa Jamhuri haukuwa na uzito wa kuwatia
hatiani na pia adhabu iliyotolewa ilikuwa ni kubwa.
Katika rufaa hiyo, Jaji wa Mahakama
hiyo, Salvatory Bongole aliieleza Mahakama kuwa hataweza kuendelea na
kesi hiyo kwa sababu mmoja wa waliokata rufaa anafahamiana naye.
Kesi hiyo itasikilizwa Julai 31 mwaka huu kwa sababu anayetarajia kuiendesha atatoka nje ya mkoa wa Dar es Salaam.
Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani
hapo kwa mara ya kwanza mwaka 2008 wakikabiliwa na mashitaka ya
kuisababishia serikali hasara ya kiasi hicho cha fedha kutokana na kutoa
msamaha wa kodi kwa Kampuni ya kukagua madini ya dhahabu ya Uingereza.
.
Hakuna maoni