WAFANYAKAZI SHIRIKA LA POSTA WATAKIWA KUBADILISHA MTAZAMO
Na Zainab Nyamka, Michuzi TV
SHIRIKA la Posta Tanzania (TPC) limewataka wafanyakazi wake kubadilisha mtazamo wao na kuendana na mfumo wa kidigitali.
Hayo yamesemwa na Kaimu Meneja Mkuu Uendeshaji Biashara Constantine Kasese alipokuwa akizungumza na wafanyakazi wa Shirika la Posta Mkoa wa Morogoro.
Kasese amesema, wafanyakazi wanatakiwa waendane na mikakati ya serikali ili kuboresha huduma ndani ya taasisi.
Amesema, Serikali imewekeza fedha nyingi ndani ya taasisi ili kuboresha mfumo wa kidigitali na hilo linaenda kuongeza mapqto ndani ya taasisi na hata serikali.
Kasese amesema,wafanyakazi pia wanatakiwa kuboresha utendaji wao wa kazi hasa maeneo yanayolegalega upande wa usafirishaji kwa kusafirisha barua na vifurushi kwa usahihi na kuongeza mapato ndani na nje ya nchi.
Ameeleza kuwa, mameneja wa mikoa watumie rasilimali zao kuwafikia wananchi na kuwapatia elimu ya huduma zinazopatikana ndani ya Shirika hilo ili kuongeza wigo wa upatikanaji wateja.
“Kuna huduma zimerahisishwa ikiwemo Huduma mpya ya Virtual Box ambayo namba yako ya simu ndiyo sanduku lako la Posta, Posta Kigangani na kuna huduma zingine zinakuja na zote zitapatikana ndani ya Shirika la Posta.”
Akizungumzia kuelekea Kilele cha Siku ya Posta duniani Oktoba 9 mwaka huu, Kasese amesema kwa mwaka huu maadhimisho hayo yatafanyika Jijini Dodoma na kila mkoa watatakiwa washiriki katika shughuli mbalimbali kuelekea siku hiyo.
Aidha, amesema kwa Mwaka huu mgeni rasmi anatarajiwa kuwa ni Makamu wa Rais Dkt Philip Mpango na tayari wanaenda kuweka historia mpya ndani ya muda mfupi toka kuanzishwa kwa Shirika hilo mwaka 1994 baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuzindua Huduma Pamoja mwanzoni mwa wiki hii.
Ameongeza, maadhimisho hayo yataanza Oktoba 4-9 na kutakuwa na mashindano yatakayokuwa yanaendelea na Mkoa utakaofanya vizuri utapatiwa zawadi kama hamasa.
Hakuna maoni