Makamu Wa Kwanza Wa Rais Amuaga Jaji Sumbu.
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, leo ameungana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi katika mazishi ya jaji Mkaazi wa Mahakama Kuu Pemba marehemu Haji Omar Haji (Sumbu).
Jaji Haji aliefariki dunia Jana katika hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja Mjini Zanzibar alikolazwa akipatiwa matibabu baada ya kuugua kwa muda mfupi, amezikwa huko Shakani Wilaya ya Magharib ‘B’ Unguja.
Miongoni mwa viongozi wengine wakitaifa walioshiriki katika mazishi hayo ni pamoja Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdalla, Mawaziri mbali mbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe. Omar Othman Makungu, Majaji wa Mahkama Kuu ya Zanzibar na mahakimu wa mahakhama za Mikoa, wilaya na viongozi wengine mbali mbali wa chama na Serikali.
Jaji Haji ambaye alianza kazi kama karani wa Mahkama Zanzibar mwaka 1996 na baadae kuteuliwa kuwa Hakimu wa Mahkma ya Mkoa Vuga mwaka 2005 hadi mwaka 2009 baada ya kuhitimu shahada ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU).
Aidha aliteuliwa kuwa Naibu Mrajis wa Mahkama Kuu Zanzibar kuanzia mwaka 2009 hadi mwaka 2011 hadi alipoteuliwa kuwa Jaji wa Mahkama kuu ya Zanzibar mwaka 2021, wadhifa ambao ameutumika hadi alipofariki dunia jana.
Jaji Haji alizaliwa katika Kijiji cha Mafia Mkoa wa Pwani, Tanzania Bara, alikoanza Masomo yake ya Msingi na baadae mwaka 1985 alihamia Zanzibar na kuendelea na masomo katika ngazi mbali mbali .
Na hadi anafariki dunia jana Septemba 11, ameacha kizuka mmoja na watoto wanne , Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi amin.
Kitengo cha Habari
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Hakuna maoni