Watu 20 wafariki kwenye meli baada ya kuwaka moto Kinshasa
Watu 20 wamefariki dunia na wengine 11 wameungua vibaya wakati meli moja iliposhika moto katika bandari ya Kinshasa, Jumapili hii.
Akizungumza na kituo cha habari cha Top Congo FM, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kinshasa, Didier Tenge Litho, amesema ajali hiyo ilitokea majira ya saa 7 mchana kwenye Bandari ya Ngafura, nje kidogo ya mji mkuu Kinshasa, katika mto Kongo.
Papy Epiana, mbunge wa jimbo hilo anayeaminika kuwepo wakati wa ajali hiyo ikitokea alisema meli iliyowaka inaitwa MB Bera iliyokuwa na shehena ya bidhaa zinazoshika moto zilizokuwa zikitoka Kinshasa kwenda jimbo la Équateur.
Waziri huyo wa Mambo ya Ndani amethibitisha kuwa watu 11 walikimbizwa hospitali ya karibu wakiwa wameungua karibu robo tatu ya sehemu zao za mwili na kupiga marufuku mizigo na abiria kusafirishwa pamoja nchini humo.
Mto Congo ni njia rahisi kwa wakongo wengi kuitumia na wanayoweza kuimudu katika nchi hiyo ya pili kwa ukubwa barani Afrika, ukubwa unaokaribia na Ulaya Magharibi, lakini ikiwa na miundombinu duni.
Kuna wakati abiria hulazimika kusubiri kwa siku kadhaa na wakati mwingine mpaka wiki kadhaa kabla ya kupata usafiri kwenye Mto Kongo na vijito vyake.
Ukosefu wa usafiri wa uhakika hulazimisha abiria kupanda usafiri wowote ambao mwingi unakua na usalama mdogo kutokana na kutokidhi vigezo vya kiusalama.
Kaika kipindi cha miezi mitano iliyopita, watu wasiopungua 55 walifariki dunia wakati boti iliyojaza abiria kuliko uwezo wake kuzama kwenye mto Kongo, katika Jimbo la Mongala Kaskazini mwa DRC, Redio Okapi, Redio ya Umoja wa Mataifa iliripoti
Hakuna maoni