Waziri Nape ayafungulia magazeti haya manne
SERIKALI imeyafungulia rasmi magazeti ya Mwanahalisi, Mawio, Mseto na Tanzania Daima yaliyokuwa yamefungiwa kwa muda mrefu.
Uamuzi huo umetangazwa leo Februari 10, 2022 na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari na kutoa leseni za magazeti hayo.
Akizungumza mara baada ya kupokea leseni za magazeti yake ambayo ni Mwanahalisi na Mseto, Said Kubenea ambaye ni mmiliki wa magazeti hayo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu kwa kufungua ukurasa mpya na vyombo hivyo vya habari huku akisisitiza kuwa wataendelea kushirikiana na Serikali.
“Agizo la Rais ni sheria na inapaswa kutekelezwa, leo nitatoa leseni kwa magazeti manne yaliyokuwa yamefungiwa ambayo ni Mwanahalisi, Mawio, Mseto na Tanzania Daima kwa sababu ni vizuri kuondoka kwenye maneno tufanye vitendo hivyo tuanze na ukurasa upya sasa mwenye maneno yake aseme mwenyewe, kifungo kimetosha kikubwa kazi iendelee,” -Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye
Hakuna maoni