Mganga Wa Jadi Atuhumiwa Kusababisha Mauaji Ya Watu Wawili Waliomfuata Kutafuta Utajiri
Watu wawili waliofahamika kwa majina ya Suzana Mtitu (38) na Kassim Kitamkanga (35) wakazi wa mjini Makambako mkoani Njombe wamekutwa wamefariki katika msitu wa Tanwat uliopo mjini Njombe.
Kamanda wa polisi mkoa wa Njombe Hamis Issah amesema watu hao wamekutwa kwenye msitu wa kupandwa wa Tanwat uliopo mjini Njombe huku sababu kubwa mara baada ya uchunguzi ikibainika kuwa ni kutokana na kuuawa na mganga wa jadi aliyetekeleza mauaji hayo baada ya watu hao waliokuwa wateja wake wa utajiri kugundua dawa walizopewa kushindwa kufanya kazi.
Kamanda Issah amesema jeshi hilo linamshikilia mganga wa kienyeji aliyefahamika kwa jina la Joseph Mgunda (41) mkazi wa Sovi kata ya Mtwango wilayani Njombe kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo.
“Watu wengi wafanyabiashara huyu mganga anawaambia ukipeleka hela anaziombea halau baadaye zinaongezeka,sintofahamu iliyotokea kwa hawa watu wawili walipewa dawa tayari lakini wakaona matokeo hayaleti mafanikio wakaenda kumuuliza mganga mbona umetupa dawa ambayo haisaidii”alisema Kmanda Issah
Issah amesema mganga huyo alishikwa na hofu na kushauriwa na ndugu zake kutekeleza mauaji hayo.
“Ndugu zake wakamwambia ukitaka usipate shida ni kuwapoteza na kweli watu watatu nayeye mwenyewe mganga wanne na wengine bado hatujawakamata wakatekeleza mauaji.Mwanaume alikatwa mapanga sehemu za shavuni upande wa kulia na kushoto na kichwani na pia kapigwa rungu na kudondoka na mwanamke alipgwa rungu moja tu na kudondoka chini”alisema Issah
Kamanda Issah amesema watu wengine wanaoshikiliwa kwa tuhuma za mauaji hayo ni pamoja na Adrew Vahuruka mkazi wa Mtwango,Gadi Mwanzalila (36) mkazi wa Igima na Kelvin Kilinge (29) Mkazi wa Igima.
Aidha ametoa wito kwa wanchi kutafuta pesa kwa juhudi za kufanya kazi na sio kutafuta utajiri kwa waganga kwa kuwa hakuna utajiri unaoletwa na waganga.
Hakuna maoni