Agizo la Rais Magufuli kuhusu kununuliwa vitanda hospitali ya Muhimbili latekelezwa
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema fedha hizo zimefanikisha kupatikana vitanda 300 vya wagonjwa pamoja na magodoro yake, shuka 600, Baiskeli za kubebea wagonjwa na vifaa vingine na kwamba hivyo vyote tayari vimepelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Balozi Sefue ameuagiza uongozi wa Hospitali hiyo kuhakikisha vitanda vyote vinafungwa jumapili na kwamba atakwenda kuvikagua siku ya jumatatu vikiwa tayari vinatumiwa na wagonjwa waliokua wanakosa vitanda vya kulalia na kulazimika kulala chini.
Wadau mbalimbali walichanga fedha kiasi cha shilingi milioni 225 kwa ajili ya kugharamia hafla ya wabunge baada ya uzinduzi rasmi wa bunge la 11 lakini Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli aliagiza fedha hizo zitumiwe kwa kiasi kidogo kisichozidi shilingi milioni 15 na nyingine zipelekwe hospitali ya Muhimbili kutatua tatizo la uhaba wa vitanda.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano IKULU,
Novemba 21, 2015.
Hakuna maoni